KITAIFA

Kauli ya Pinda yaonyesha udhaifu’Baadhi ya wanasiasa na wanaharakati wamemkosoa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kutokana na kutamani kung’olewa kwenye nafasi, wakidai kuwa kauli yake inaonyesha jinsi alivyo mpole na dhaifu kiutendaji .

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba ayezungumza na gazeti hili jana kwa njia ya simu alisema kuwa kauli ya Waziri Mkuu Pinda imeonyesha kwamba ana tatizo la kutokujiamini.
“Kazi za Waziri Mkuu zinajulikana wazi kwamba ni majukumu mazito ikiwemo kusimamia utendaji wa Serikali kwa kila wizara, hivyo kusema asihukumiwe kwa sababu ya wizara chache zisizofanya vizuri, inaonyesha ameshindwa majukumu yake. Alichotakiwa kufanya kwa wizara hizo ni kumshauri Rais awaondoe madarakani wasiowajibika,” alisema.
Alisisitiza: “ Hatutegemei kumwona Waziri Mkuu akiingia kufanya kazi kwenye kila wizara, isipokuwa anatakiwa kumshauri Rais ili mambo yaende sawa.” Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro, alisema kuwa amekuwa akifuatilia kauli za Waziri Mkuu Pinda hata anapokuwa kwenye ziara za kikazi, ambapo amekuwa akitoa kauli za kuwabembeleza watendaji, hata wanapoboronga.


Familia ya Nyerere yaenda Qunu kumzika Mandela







Familia ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere itawakilishwa katika mazishi ya Rais wa Kwanza Mzalendo wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, ambaye atazikwa kesho katika Kijiji cha Qunu, Mthatha Jimbo la Eastern Cape.
Habari ambazo gazeti hili lilizipata jana mjini Pretoria zinasema kuwa Mama Maria Nyerere, ambaye ni mjane wa Baba wa taifa, alialikwa kuhudhuria mazishi hayo kwa kuzingatia uhusiano uliopo baina ya familia hizo mbili.
Hata hivyo, imethibitika kuwa Mama Maria hataweza kuhudhuria mazishi hayo kesho, badala yake amewatuma wawakilishi ambao ni mabinti zake wawili; Anna Nyerere ambaye ni mtoto wa pili na mtoto wake wa saba, Rosemary Nyerere.
Madaraka Nyerere ambaye ni mtoto wa sita wa Mwalimu alithibitisha jana kwamba familia yao imealikwa kushiriki mazishi hayo, lakini akaweka wazi kwamba: “Mama hataweza kwenda kuzika, atakwenda baadaye kidogo baada ya mazishi kufanyika.”
Madaraka alisema kwa jinsi afya ya mama yake ilivyo sasa, hataweza kwenda Qunu. “Kwa kawaida mazishi haya ya kitaifa huwa yana mambo na pilika nyingi, kwa hiyo mama ameona asubiri,” alisema.

Dk Kawambwa ajibu makombora ya NapeWaziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa amejibu madai yaliyotolewa hivi karibuni na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye kwamba ni mmoja wa mawaziri walioshindwa kazi, hivyo kustahili kung’olewa.

Katika madai yake, Nape alisema Dk Kawambwa ameshindwa kusimamia vyema madai ya walimu na kwamba akiwa Waziri wa Miundombinu, aliingia mkataba na Kampuni ya ujenzi ya Progressive iliyopewa zabuni ya kujenga Barabara ya Namtumbo hadi Tunduru wakati mkandarasi huyo hana uwezo wa kuijenga.
Nape alikaririwa akisema kwamba umefika wakati kwa waziri huyo na wenzake wa Fedha, Dk William Mgimwa; Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza; na Naibu wake, Adam Malima kuhojiwa na Kamati Kuu (CC) ya chama hicho.



Kairuki ataka ushirikiano kuukabili unyanyasaji 

 

Washiriki mbalimbali wa maendeleo na wadau wa masuala ya jinsia wametakiwa kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia vinafikia tamati.

Rai hiyo imetolewa jijini Dar es salaam na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angellah Kairuki wakati akizindua siku 16 za kupinga ukatili na unyanyasaji wa kijinsia.
Sambamba na uzinduzi huo Kairuki alizindua pia mfumo wa utoaji wa huduma kwa mfumo wa One Stop Center ambao unajumuisha huduma zote muhimu kwa watakaokutana na ukatili wa kijinsia kama vile polisi, afya na ustawi wa  jamii kutolewa sehemu moja.

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni