Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Chadema kimesema kwamba kilifikia uamuzi wa kumvua nyadhifa zake, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wake, Zitto Kabwe kutokana na sababu moja tu ya kuhusika katika Waraka wa Mkakati wa Mabadiliko 2013.
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu
aliwaambia waandishi wa habari Dar es Salaam jana kwamba waraka huo
unaeleza mbinu za uasi ambazo zililenga kufanya mabadiliko makubwa ya
kiuongozi wakati wa uchaguzi mkuu wa ndani wa chama hicho jambo ambalo
ni kinyume na katiba, sheria na itifaki za Chadema.
Hivi karibuni, Kamati Kuu ya Chadema iliwavua
nyadhifa zao, Zitto, Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo na
Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba kutokana na madai hayo.
Siku tatu zilizopita, Zitto na Dk Kitila
waliitisha mkutano wa wanahabari na kueleza sababu mbalimbali za
kung’olewa kwao ikiwamo suala la posho na ruzuku za vyama vya siasa.

Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imepiga marufuku biashara ya kutembeza visu, sime na mapanga barabarani na kusema yeyote atakayekiuka agizo hilo atakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Polisi yapiga marufuku kuuza visu, sime, mapanga barabarani
Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imepiga marufuku biashara ya kutembeza visu, sime na mapanga barabarani na kusema yeyote atakayekiuka agizo hilo atakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi
Kanda hiyo, Kamishna Suleiman Kova alisema jeshi hilo lipo katika
mchakato wa kupendekeza sheria mpya ya matumizi ya silaha na umiliki ili
kudhibiti matumizi mabaya yakiwamo uuzaji wa visu, mapanga na sime
kiholela.
Kamishna Kova alisema tatizo kubwa si mtu kumiliki
silaha, bali jinsi watu wanavyozitumia vibaya na kusababisha madhara
katika jamii na kuongeza kuwa sheria hiyo itajumuisha uuzaji holela wa
visu, mapanga na sime barabarani na umiliki wa silaha za moto.

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, imepeleka mapendekezo ya kuboresha sheria 32 serikalini tangu ilipoanzishwa mwaka 1983, lakini zilizofanyiwa kazi ni 13.
Tume ya Sheria ‘yalilia’ mapendekezo yake
Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, imepeleka mapendekezo ya kuboresha sheria 32 serikalini tangu ilipoanzishwa mwaka 1983, lakini zilizofanyiwa kazi ni 13.
Akitangaza maadhimisho ya miaka 30 tangu
kuanzishwa kwa tume hiyo jana, Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria
Tanzania, Jaji Aloysius Mujulizi alisema hiyo ni changamoto kwao kwa
sababu tume haina kipengele cha sheria kinachoiruhusu kuhoji Serikali
kama mapendekezo yake hayajafanyiwa kazi. Jaji Mujulizi alisema miongoni
mwa kazi za tume hiyo ni kufanya mapitio ya sheria na kupendekeza, ili
zifanyiwe marekebisho kulingana na mahitaji ya watu na wakati uliopo.
Alizitaja baadhi ya sheria zilizotungwa kutokana
na kazi ya Tume hiyo kuwa ni, Sheria ya Kazi ya mwaka 2004 na Sheria ya
Mtoto ya mwaka 2009.
Nyingine ni Sheria ya Usimamizi wa Vinasaba vya
Binadamu ya mwaka 2009 na kutungwa kwa kanuni mpya za Mahakama ya Rufaa
ya mwaka 2009.
Jaji Mujulizi alisema kazi nyingine zinazofanywa
na tume hiyo ni kufanya tafsiri za sheria mbalimbali kutoka lugha ya
Kiingereza kwenda Kiswahili.
“Kutokujua sheria haiwezi kuwa kinga kwa
anayeivunja, hivyo tumekuwa tukitafsiri sheria mbalimbali ili wananchi
waweze kuwa na uelewa na hivyo kuzifuata,” alisema.
Alitaja baadhi ya sheria zilizotafsiriwa kuwa ni
Sheria ya Mikataba, Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini, Sheria ya Kuzuia
Fedha Haramu na Sheria ya Usimamizi wa Mirathi.
Kuhusu maadhimisho hayo, Jaji Mujulizi alisema
Rais Jakaya Kikwete kesho atafungua mkutano utakaohusisha wadau wa
sheria kutoka ndani na nje ya sheria utakaofanyika Dar es Salaam.
Alisema wananchi wana jukumu la kutoa michango kwa tume hiyo kila
wanapobaini sheria ambazo hazifai ili zifanyiwe marekebisho.
“Hizi ni sheria za wananchi hivyo wananchi wasikae
mbali na tume yao, watoe mapendekezo yao ili yafanyiwe kazi kwa lengo
la kuboresha,” alisema Jaji Mujulizi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni