Jumamosi, 14 Desemba 2013

Hali tete baraza la mawaziri


Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM chini ya Mwenyekiti wake Rais Jakaya Kikwete, imeanza kuwahoji mawaziri waliotajwa ni ‘mzigo’ kwa Serikali.
Hata hivyo, habari za ndani zilieleza kwamba miongoni mwa ajenda kuu za CC ni kuwahoji mawaziri wanaolalamikiwa na wananchi, kwamba wameshindwa kutekeleza majukumu yao.



Maelfu wakwama kumuaga Mandela

 
Maelfu ya wananchi wa Afrika Kusini wameshindwa kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa Rais wa Kwanza mzalendo wa nchi hiyo, Nelson Mandela kutokana na muda uliopangwa kumalizika.
Kuanzia Jumatano wiki hii hadi jana, mwili wa Mandela aliyefariki dunia Desemba 4 mwaka huu, ulikuwa ukiwekwa katika Ikulu ya Pretoria, iliyopo ndani ya Majengo ya Umoja (Union Buildings), kila asubuhi kwa ajili ya wananchi kutoa heshima za mwisho.
Jana ilikuwa siku ya mwisho ya utoaji wa heshima hizo na hadi muda uliowekwa ulipokwisha saa 11:30 jioni, kulikuwa na maelfu ya watu waliokosa fursa ya kumuaga mpendwa wao huyo.
Dalili za idadi kubwa ya watu kukosa nafasi hiyo adhimu zilianza kuonekana Jumatano na baadaye juzi Alhamisi kwani hadi muda wa kufunga ulipofika jioni, maelfu ya watu walirejea nyumbani bila kupata fursa ya kuaga.
Jana mchana, Serikali ilitoa taarifa kwamba kwa kuzingatia idadi ya watu waliojitokeza kutoa heshima zao za mwisho, ilikuwa vigumu kwa watu wote kufikiwa.




Lowassa anusurika ajali ya ndege Arusha



Abiria 37 waliokuwa wamesafaria ndege ya Shirika la Precision Air, akiwamo Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, jana walinusurika kifo, baada ya magurudumu manne ya ndege hiyo kupasuka ilipokuwa ikitua katika Uwanja wa Ndege wa Arusha.
Tukio hilo la aina yake, lilitokea saa 6:15 mchana, wakati ndege hiyo, ikitua kutoka jijini Dar es Saalam, ikiwa na abiria hao 37, marubani wawili na wahudumu wawili.
Kamanda wa polisi mkoani Arusha, Liberatus Sabas alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kueleza hakuna majeruhi aliyeripotiwa.
“Hadi sasa hali ni shwari, ndege iliweza kusimama licha ya kupasuka magurudumu. Kiutaratibu uchunguzi umeanza kufanywa na wataalamu husika,”alisema Kamanda Sabas.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni