Wakili wa kujitegemea na Diwani wa Kata ya Mabogini mkoani Kilimanjaro (Chadema), Albert Msando ameeleza kasoro nne za kisheria ambazo zimefanywa na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu wakati wa kutoa hukumu kwa makosa yaliyofanywa na makada wa chama hicho, Zitto Kabwe na Dk Kitila Mkumbo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Msando
alisema Katiba ya Chadema inaeleza kuwa kiongozi yeyote hatachukuliwa
hatua za kinidhamu kabla ya kupewa mashtaka kwa maandishi na mamlaka
husika na kupewa nafasi ya kujibu mashtaka hayo kwa maandishi.
“Tunaomba Lissu aeleze kwa njia ileile aliyotumia kueleza umma
wa Watanzania uamuzi wa Kamati Kuu, siku na tarehe ambayo Dk Kitila na
Zitto walipewa mashtaka yao kwa maandishi na atoe nakala ya majibu yao
kwa maandishi kama yapo kwa mujibu wa Katiba ya Chadema,” alisema na
kuongeza:
“Aeleze ni utaratibu gani ulitumika kuwajadili
kwenye kikao cha Kamati Kuu, kufikia uamuzi na kuwapa adhabu ya kuwavua
madaraka wakati hawajapewa mashtaka hayo kwa maandishi kama Katiba
inavyosema, kisha Kamati Kuu kwenda kwenye vyombo vya habari na kueleza
kuhusu uamuzi huo na kutoa siku 14 ili wajieleze.”
Alisema Lissu hatakiwi kutoa majibu ya jumla, bali
kueleza utaratibu, sheria na utawala bora gani uliotumika kuchukua
uamuzi huo dhidi ya Zitto na Dk Kitila. Alisema Lissu pia anatakiwa
kueleza aina ya ushahidi alionao ambao ulitumika kuwahukumu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni